Thursday, February 21, 2013

sababu 21 za kumfanya muislam asisherekee maulid

Sababu 21 Za Kumfanya Muislam Asisherehekee Maulidi

BismiLLaah wa-AlhamduliLLaah was-Swalaatu was-salaam 'alaa Muhammad wa 'alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba'ad

Zifuatazo ni sababu na hoja ambazoMuislam mwenye kupenda kufuata haki na mwenye kutaka apate uongofu ili abakie katika njia iliyonyooka na ajiepushe na mambo ya baatil. Hoja ni za wazi kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Hoja za kupinga jambo hili ziko nyingi sana, lakini tulizozikusanya tunatumai kuwa zitamtosheleza Muislamu aikinaishe nafsi yake kuwa Maulidi ni jambo la uzushi katika dini kwa hiyo ni bora kutenda amali zile tulizopata mafundisho yake kutoka kwa Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم, Maswahaba wake na Salafus Swaalih (Watangu wema).

 

 

SABABU YA KWANZA:

Kumpenda Mola Mtukufu Aliyetuumba 

Kwanza kabisa ni kwa sababu  ya kumpenda Mola Mtukufu Aliyetuumba Ambaye Anataka kuhakikisha kuwa mapenzi yetu Kwake ni kumfuata Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye tokea kuzaliwa kwake hadi kufa kwake hakufanyiwa wala hakusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

 

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

 ((قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ)) 

((Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu)) [Al-'Imraan: 31] 

 

 

SABABU YA PILI:

Kufuata amri yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم    ya kushikamana na Sunnah Zake na Sunnah za Makhalifa wake

 (( أُوصِيكُمْ بِتَقْوى اللَّه، وَالسَّمْعِ وَالطَّاعَةِ وإِنْ تَأَمَّر عَلَيْكُمْ عَبْدٌ حبشيٌ ، وَأَنَّهُ مَنْ يَعِشْ مِنْكُمْ فَسَيرى اخْتِلافاً كثِيرا . فَعَلَيْكُمْ بسُنَّتي وَسُنَّةِ الْخُلُفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ ، عضُّوا عَلَيْهَا بالنَّواجِذِ ، وإِيَّاكُمْ ومُحْدثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٍ ضلالَةٌ ))  رواه أبو داود ، والترمذِي وقال حديث حسن صحيح

((Nakuusieni kumcha Allaah, usikivu na twaa hata ikiwa kiongozi wenu (Au atakayekuamrishen) ni Mtumwa  wa Habash. Mtakaoishi miongoni mwenu mtaona ikhtilafu nyingi. Kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waliongoka baada yangu.  Ziumeni kwa magego (zikamateni kwa nguvu wala msiziache). Na tahadharini na mambo ya uzushi kwani kila bid'ah ni upotofu)) [Abu Daawuud, At-Trimidhiy kasema Hadiyth Hasan Swahiyh]   

Kwa hiyo inamtosheleza Muislamu hoja hii pekee ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wala Maswahaba zake hawakusherehekea Maulidi, kumfanya naye asisherehekee.

Na hiyo ndio sababu kubwa ya Waislamu kukhitilafiana na kugawanyika makundi makundi. Amesema Imaam Maalik رحمه الله "'Hakuna kitakachotengeneza Ummah huu wa mwisho ila kwa kile kilichotengeneza Ummah wa mwanzo". Na maadam Salafus-Swaalih (watangu wema) hawakufanya bid'ah kama hii, sisi ni lazima tuwe na khofu kubwa ya kuifanya.

 

 

SABABU YA TATU

Ametuamrisha Allaah سبحانه وتعالىtufuate aliyotuletea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na tujiepushe na aliyotukataza  

 ((وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا))

((Na anachokupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho)) [Al-Hashr: 7]

 

 

SABABU YA NNE:

Kufuata amri ya Kumtii Allaah سبحانهوتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم

Anasema Allaah سبحانه وتعالى katika Aayah nyingi kwenye Qur-aan:

((وَأَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ))

((Na mtiini Allaah na mtiini Mtume ))[At-Twaghaabun: 12]

Na kumtii Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kumtii Allaah سبحانه وتعالى

((مَّنْ يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللّهَ))

((Mwenye kumtii Mtume basi ndio amemtii Allaah)) [An-Nisaa: 80]

 

 

SABABU YA TANO:

Kutokufuata amri ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ni kumkhalifu na kupata adhabu kali 

 ((فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيم))

((Basi nawatahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu)) [An-Nuur: 63]

 

 

SABABU YA SITA

Kumpinga Mtume صلى الله عليه وآله وسلمni sababu ya kuingizwa motoni

 ((وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَى وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّى وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ وَسَاءتْ مَصِيرًا))

((Na anayempinga Mtume baada ya kumdhihirikia uongofu, na akafuata njia isiyo kuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannamu. Na hayo ni marejeo maovu)) [An-Nisaa: 115]

 

 

SABABU YA SABA:

Kukhofu upotofu unaompeleka mtu motoni

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Alikuwa akitanguliza khutba zake kwa kutoa maonyo hayo:

(( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد صلى الله علي وسلم  وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار))  أخرجه مسلم في صحيحه 

((Maneno bora  ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na Uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم  na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi)  na kila bid'ah ni motoni)) [Muslim katika Swahiyh yake]

 

 

SABABU YA NANE:  

Khofu ya kuwa miongoni mwa kundi litakaloingia motoni

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipoonya katika Hadiyth ifuatayo kuwa makundi yote yanayojiita ni ya Kiislam na hali hayafuati mafunzo kama aliyokuja nayo yeye, yatakuwa motoni isipokuwa kundi moja. Maswahaba walishtuka na wakataka kujua ni kundi gani hilo moja, akawajibu kuwa ni kundi ambalo watu wake watakuwa wanafuata mwendo wake na wa Maswahaba zake.

((افترقت اليهود على إحدى وسبعين فرقة، وافترقت النصارى على اثنتين وسبعين فرقة، وستفترق هذه الأمة على ثلاث وسبعين فرقة كلها في النار إلا واحدة،)) فقال الصحابة: من هي يا رسول الله؟ قال: ((من كان على مثل ما أنا عليه وأصحابي)) الترمذي و الحاكم

((Waligawanyika Mayahudi katika makundi sabini na moja, na waligawanyika Manaswara katika makundi sabini na mbili, na utagawanyika Umma wangu katika makundi sabini na tatu, yote yataingia motoni ila moja!)) Maswahaba wakasema: 'Ni kundi lipi hilo Ee Mtume wa Allaah?  Akajibu: ((Ni lile ambalo litakuwa katika mwenendo wangu hii leo na Maswahaba zangu))[Imepokewa na Maimaam At-Tirmidhiy na Al-Haakim]

 

 

SABABU YA TISA:

Kuitikia wasiya wa Allaah سبحانه وتعالى ili kubakia katika njia iliyonyooka

Anasema Allaah سبحانه وتعالى

 ((وَأَنَّ هَذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ))

((Na kwa hakika hii ndiyo Njia Yangu Iliyonyooka. Basi ifuateni, wala msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya Amekuusieni ili mpate kumcha Mungu)) [Al-An'aam: 153]

 

 

SABABU YA KUMI:

Vitendo visivyokuwa vya Sunnah havipokelewi

 (( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa chetu (katika dini yetu) basi kitarudishwa)) [Al-Bukhaariy]

Hivyo mtu atapoteza muda wake, labda na gharama ya kutekeleza bid'ah hii na kumbe amali hii haina thamani yoyote mbele ya Allaah.

 

 

SABABU YA KUMI NA MOJA:

Maulidi  yamezushwa karne ya nne (miaka mia nne) baada ya kufa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na watu wenye kufru

Walioanzisha Maulidi ni viongozi waFaatwimiyyun huko Misr (hawa walikuwa ni Rawaafidh (Mashia) katika dhehebu la Ismailiyah [Makoja] walianza kusherehekea  Maulidi ya 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu), na Maulidi ya Hasan na Husayn (Radhiya Allaahu 'anhuma), na Maulidi ya Faatwimah az-Zahraa (Radhiya Allaahu 'anha), na Maulidi ya kiongozi wao aliye hai kwa wakati ule. Sasa kwa nini tuwafuate wao? Na kamaalivyotujulisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلمkwamba watu bora kabisa wa kuwafuata ni wa karne tatu pekee aliposema:

((خير القرون قرني ثم الذين يلونهم ثم الذين يلونهم)) متفق عليه 

((Karne zilizo bora kabisa ni karne yangu, kisha inayofuatia kisha inayofuatiya)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

SABABU YA KUMI NA MBILI:

Makafiri wanafurahi Waislamu wanapofanya Bid'ah kwani ni kuacha mafunzo sahihi ya dini na ni kuzifuta Sunnah za Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

Napoleon Bonaparte alimpa Shaykh Al-Bakriy Riyaal mia  nane za Ufaransa (inasemekana ni mia tatu kwenye sehemu zingine) ili arudishe bid'ah ya Maulidi naye akahudhuria mwenyewe Maulidi. Maana makafiri wanajua kuwa Waislam wanaposhughulishwa na vipumbazo kama hivyo, husahau matakwa yao ya msingi na muhimu.

 

 

SABABU YA KUMI NA TATU:

Baadhi ya maneno katika Maulidi yana kufru ya kumpandisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم cheo cha usawa na Allaah سبحانه وتعالى wakati yeye ametuonya tusifanye hivyo

 ((لا تطروني كما أطرت النصارى المسيح ابن مريم، إنما أنا عبد، فقولوا: عبد الله ورسوله))  متفق عليه

((Msinitukuze Kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi na mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Mjumbe Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

SABABU YA KUMI NA NNE

Wanapoinuka kumswalia Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم wanaamini kwamba roho yake inahudhuria wakati huo

Hii ni fikra ovu kabisa, na pia yeye mwenyewe alikuwa hapendi kuinukiwa alipokuwa hai, vipi mtu anayempenda amfanyie jambo analolichukia wakati amekufa?

Siku moja Maswahaba walikuwa wamekaa msikitini pamoja na Abubakar رضي الله عنه ambaye alikuwa akisoma Qur-aan. 'Abdullah ibn Ubbay ibn Saluul, mnafiki mkubwa alikuja akaweka takia na mto wake akaketi. Alikuwa ni mwenye sura nzuri na mwenye lugha ya ufasaha. Alisema: "Ewe Abu Bakar, muulize Mtume صلى الله عليه وآله وسلم atuonyeshe alama ya utume wake kama walivyotuonyesha Watume wengine. Mfano, Muusa عليه السلام  ametuletea Ubao (wa Tauraat), 'Iysa عليه السلام alituletea Injiyl na meza ya chakula kutoka mbinguni, Daawuud عليه السلام alituletea Zabuur, Swaalih عليه السلام alitulietea ngamia wa kike" Abu Bakar رضي الله عنه aliposikia akaanza kulia. Mara akaingia Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم na Abu Bakar رضي الله عنه akawaambia Maswahaba wengine wainuke kumpa heshima Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na kumpa malalamiko ya mnafiki. Mtume صلى الله عليه وآله وسلمakasema: ((Sikizeni! Msiniinukie mimi bali….

وَقُومُواْ لِلّهِ قَانِتِينَ

((na simameni kwa ajili ya Allaah)) [Al-Baqarah: 238] (dalili kutoka Tafsiyr Ibnu Kathiyr]

 

 

SABABU YA KUMI NA TANO:

Kuchanganyika kwa wanawake na wanaume

Jambo ambalo limekatazwa katika dini na katika sherehe hii kumedhihirika sana hasa pande za nchi zetu za Afrika Mashariki. Na uovu huu unafikia hadi kuimba kwa pamoja na kuchezesha vichwa kama kwamba ni dansi fulani. Imefika hadi maulidi kuitwa 'disco maulidi'

 

 

SABABU YA KUMI NA SITA

Kuwaigiza Manaswara

Manaswara wanasherehekea siku ya kuzaliwa 'Iysa عليه السلام kama wanavyodai. Na Waislamu haitupasi kusherehekea siku ya kuzaliwa  Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kwani tumefundishwa kuwa tufanye kinyume na wao katika mambo yetu.

Vilevile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kasema:

 ((خالفوا المشركين، أحفوا الشوارب، وأوفوا اللحى))البخاري و مسلم

((Kuweni kinyume na Washirikina, punguzeni masharubu na fugeni ndevu)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na kufanya hivyo (kusherehekea Maulidi) tutakuwa tunajifananiza nao, na jambo hilo la kuwaiga na kujifananisha na mambo yao limekatazwa kama alivyosema Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم:

 ((من تشبه بقوم فهو منهم )) أحمد و أبو داود

Anayejishabihisha na watu basi naye ni miongoni mwao)) [Ahmad, Abu Daawuud]

 

 

SABABU YA KUMI NA SABA:  

Dini imekamilika hakuna tena haja ya kuleta mambo ya dini mapya

Kuzusha mambo mapya ya dini ni kama kumtuhumu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuwa ametukhini mafunzo ya dini na hakuyakamilisha, bali kuna aliyoyaficha na hakutupa yote!! Na hali aliikamilisha dini kama ilivyompasa. Aayah hii chiniiliteremshwa kudhihirisha ukamilifu wa dini ya Mola Mtukufu

 ((الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينً))

((Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni Neema Yangu, na Nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini)) [Al-Maaidah: 3]

Sasa vipi watu walete mafundisho ya dini mapya yasiyotokana na mafunzo kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى na Mtume Wake صلى الله عليه وآله وسلم ? Anauliza Allaah سبحانه وتعالى :

((أَمْ لَهُمْ شُرَكَاء شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّهُ))

((Au hao wana miungu ya kishirikina waliowatungia dini asiyoitolea idhini Allaah?)) [Ash-Shuura 21]

 

 

SABABU YA KUMI NA NANE:

Kudhihirisha iymaan kwa kupenda yale aliyokuja nayo Mtume صلى الله عليه وآله وسلم pekee

عَنْ أَبِي مُحَمَّدٍ عَبْدِ اللَّهِ بِنْ عَمْرُو بِنْ العَاصِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وآله وسلم: ((لا يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يَكُونَ هَوَاهُ تَبَعَاً لِمَا جِئْتُ بِهِ )) حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ، رَوَيْنَاهُ فِي كِتَابِ "الْحُجَّةِ  بِإِسْنَادٍ صَحِيحٍ.   

Kutoka kwa Abu Muhammad Abdullah Ibn 'Amr Bin Al-'Aasw رضي الله عنهambaye alisema:  Mtume صلى الله عليه وسلم kasema: ((Hatokuwa kaamini (kikwelikweli) mmoja wenu mpaka mapenzi yake yatakapomili (yatakapotii au kuwafikiana) kwenye yale niliyoyaleta)) (mafundisho)[Hadiyth Hasan iliyotoka katika kitabu "Al-Hujjah" ikiwa na mtiriko mzuri wa mapokezi].

 

 

SABABU YA KUMI NA TISA:

Kuacha mambo yenye shaka na kubakia katika yaliyo wazi

 عَنْ أَبي مُحمَّدٍ الحسَنِ بْنِ عليّ بْنِ أبي طَالِب، سِبْطِ رَسُولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم وَرَيْحَانَتِهِ رضيَ اللهُ عنهُما، قالَ: حَفِظْتُ مِنْ رَسُولِ الله صلى الله عليه وسلم: ((دَعْ ما يَرِيبُكَ إلى مَا لاَ يَرِيُبكَ )) رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ   وَالنَّسَائِيُّ    وَقَالَ التِّرْمِذِيُّ: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ. 

Kutoka kwa Abu Muhammad Al-Hasan Ibn 'Aliy Ibn Abi Twaalib mjukuu wa Mtume صلى الله عليه وسلم na kipenzi chakeرَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا  alisema: "Nilihifadhi kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وسلمmaneno haya: ((Acha kile kinachokutia shaka ufuate kile kisichokutia shaka)). [Imesimuliwa naAt-Tirmidhiy na An-Nasaaiy, At-Tirmidhiy akisema kuwa ni hadiyth Hasan na Swahiyh].

 

 

SABABU YA ISHIRINI:

Mwezi huu wa Rabiy'ul Awwal ni mwezi alioaga dunia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم , sasa vipi Muislamu asherehekee?

Wanachuoni wote wameafikiana kuwa siku hii ya tarehe 12 Rabiy'ul Awwal nisiku aliyofariki Mtume صلى الله عليه وآله وسلمVipi sasa watu watakuwa wanafurahi kwa siku kama hiyo? Anas bin Maalikرضي الله عنه anatuhadithia kuwa:"Hakuna siku ambayo watu wa Madiynah walikuwa na furaha ya hali ya juu kama siku aliyohamia Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم  katika mji huo. Na hakuna siku ya huzuni kabisa kwa watu wa Madiynah kama siku aliyoaga dunia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ."

Inaonekana kama sisi tunakwenda kinyume na maadili ya wale watu bora waliokuwa wakimpenda Mtume صلى الله عليه وآله وسلم hata kuliko nafsi zao wenyewe.

 

 

SABABU YA ISHIRINI NA MOJA:  

Sababu za Waislamu wanaoshikilia Bid'ah

 

1- Kufuata bila ya kupata elimu sahihi

Ukitaka kujua hoja za Waislamu wanaofuata bid'ah, hutopata kutoka kwao hoja nyingi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, bali ni hoja za kutokana na rai zao tu, au watakwambia, 'kwani kuna ubaya gani?'. Na hata wakitoa hoja kutoka katika Qur-aan na Sunnah basi utakuta kwamba wanazifasiri dalili hizo isivyokusudiwa bali wanazishabihisha na matamanio yao kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى :

((هُوَ الَّذِيَ أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ فَأَمَّا الَّذِينَ في قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاء الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاء تَأْوِيلِه))

 ((Yeye Ndiye Aliyekuteremshia Kitabu (hiki Qur-aan). Ndani yake zimo aayah Muhkam (nyepesi kufahamika) ambazo ndizo msingi (asili) wa Kitabu (hiki). Na ziko nyingine Mutashaabihaat (zinababaisha kama habari ya Akhera, za Peponi na Motoni na mengineyo ambao yamekhusika na Roho). Wale ambao nyoyoni mwao mna upotofu wanafuata zile zinazobabaisha kwa kutaka kuwaharibu watu na kutaka kujua hakika yake vipi)) [Al-'Imraan: 7]

Na ukizingatia utaona kuwa Waislamu wanaofuata Bid'ah sio wenye elimu kubwa ya juu, kwani ukilinganisha na wanaofuata Sunnah utaona kuwa kuna tofauti kubwa sana. Na hivyo ndivyo Allaah سبحانه وتعالى Anavyomjaalia kumpa elimu ya upeo wa juu yule mwenye kufuata haki. Na tujiulize Maulamaa wangapi wacha Mungu wenye elimu madhubuti wanafuata Bid'ah? Si rahisi kuwapata, bali ukiuliza wanaofuata Sunnah na wenye elimu kubwa ambayo athari yake tunaiona leo hii na itaendelea kizazi hadi kizazi InshaAllaah, utakuta  ni wengi sana, miongoni mwao ni Maimamu wanne; Imaam Shaafi'iy, Ahmad bin Hanbali, Abu Haniyfah, Maalik, Sufyaan Ath-Thawry. Wasimulizi wa Hadiyth kina Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na kadhalika. Maulamaa maarufu; Ibn Taymiyah, ibnul Qayyim, ibnul Jawzy, ibnul Mubaarak, ibnu Hajar, ibnu Kathiyr, Imaam An-Nawawy, na waliopita katika miaka ya karibuni kama kina: ibn 'Uthaymiyn, ibn Baaz, Shaykh Al-Albaaniy na kadhalika. Hata katika jamii yetu kuna waliokuwa wamejaaliwa kupewa kipaji cha elimu kama kina Shaykh 'Abdullah Swaalih Al-Faarisy na kina Al Amiyn na Muhammad Qaasim Mazrui, Haarith Swaalih na wengineo wengi, bila kuwataja walio hai ambao hawana idadi kwa wingi wao.

 

2- Kufuata matamanio ya nafsi

Hufuata matamanio ya nafsi inavyopenda na sio kufuata haki. Wengine kutokana na unasaba wao huwa ni kwao kama utukufu kuwa nao wamo katika unasaba wa Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((وَلاَ تَتَّبِعِ الْهَوَى فَيُضِلَّكَ عَن سَبِيلِ اللَّهِ))

((Wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Allaah))[Swaad: 26]

 

3- Ugumu wa kuacha mila uliotokana na mababa na mababu

Mitume waliopita walikuwa wakiwaita watu wao wawafuate waliyokuja nayo ya haki walipendelea kubakia katika ujinga na mila za mababa zao. Na Waislamu wenye kufuata mambo ya bid'ah nao ni vile vile ukiwauliza kwa nini hamuachi mambo yasiyo katikamafundisho ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wanajibu hivyo hivyo kuwa 'vipi tuache Maulidi na hali tumekulia nayo?, au tutaachaje kitu ambacho mababa zetu walikuwa wakifanya?? Ina maana wao walikuwa hawajui?"

Anasema Allaah سبحانه وتعالى:

((وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْاْ إِلَى مَا أَنزَلَ اللّهُ وَإِلَى الرَّسُولِ قَالُواْ حَسْبُنَا مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءنَا أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لاَ يَعْلَمُونَ شَيْئًا وَلاَ يَهْتَدُون))

((Na wanapoambiwa: Njooni kwenye yale Aliyoyateremsha Allaah, na kwa Mtume, husema: Yanatutosha tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka?)) [Al-Maaidah: 104]

Au walikuwa wakisema:

((بَلْ قَالُوا إِنَّا وَجَدْنَا آبَاءنَا عَلَى أُمَّةٍ وَإِنَّا عَلَى آثَارِهِم مُّهْتَدُونَ))

((Bali wanasema: Hakika sisi tuliwakuta baba zetu wanashika dini makhsusi, basi na sisi tunafuata nyayo zao)) [Az-Zukhruf: 22]

 

4- Kukhofu kutokuungana na wengi wanaofuata bid'ah

Wengine ukiwauliza kwa nini unafuata bid'ah ya Maulidi. Jibu ni kuwa anakhofu kuwa yeye peke yake ataonekana kuwa hasomi Maulidi katika kundi lake, na hii ni hatari ya kukhofu watu badala ya kumkhofu Mola Mtukufu na pia ni kwenda na mkumbo kwa kudhani kuwa wengi ndiyo wenye haki! Haya Anatueleza Allaah kuwa:

((وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللّهِ إِن يَتَّبِعُونَ إِلاَّ الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلاَّ يَخْرُصُونَ))

((Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Allaah. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu)) [Al-An'aam: 116]

 

5- Wengine wanasema kuwa ni kudhihirisha mapenzi ya Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم

Je, mapenzi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  yadhihirike siku moja tu? Au katika mwezi huu tu? Na si siku zote? Hayo bila shaka ni mapenzi ya uongo. Mapenzi ya kweli ni yale ya kumkumbuka siku zote na kumtii umpendaye. Haya ya Maulidi hayana moja kati ya mawili hayo.

6- Hoja ya kusema ni Bid'atun-hasanah (uzushi mzuri)

Mojawapo yao ni kuwa Maulidi ni Bid'atun-hasanah. Katika dini ya Kiislamu hakuna bid'ah nzuri kwani Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   alipotuonya alisema 'Kullu Bid'atin Dhwaalaah' (kila bid'ah ni upotofu). Na ikiwa kauli hii wanaipinga kuwa sio  KILA bid'ah, basi wanasemaje kuhusu kauli ya Allaahسبحانه وتعالى Anaposema:

 ((كُلُّ نَفْسٍ ذَآئِقَةُ الْمَوْتِ))

((Kila nafsi itaonja mauti)) [Al-'Imraan: 185]

Je, tupinge pia kauli hii kuwa sio KILA nafsi? Na je, ina maana kuwa kuna watu wengine watabakia hawatokufa na hali tunatambua kuwa hakuna atakayebakia ila Mwenyewe Mola Mtukufu?

Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuhidi kwa kutuonyesha yaliyo haki ili tuyafuate na Atuonyeshe yaliyo baatil tujiepushe nayo. Aamiyn.

No comments: