بسم الله الرحمن الرحيم
Ndoa katika Uislamu ni ibada kama zilivyo ibada nyingine, zimepata mwongozo kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na Mtume (صلى الله عليه وسلم). Ndoa pindipo ikifungwa inatakiwa itangazwe hadharani na isifanywe kisirisiri. Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم):
'أعلنوا النكاح' رواه أحمد والحاكم وصححه
"Itangazeni ndoa." [Imepokewa na Imaam Ahmad na Al-Haakim, na ameisahihisha].
Na katika jumla ya kutangaza Ndoa ni kufanya yafuatayo:
1. Kufungwa Mkataba wa ndoa ('Aqd) hadharani na kushuhudiwa kwa uchache na mashahidi wawili waadilifu. Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم):
لانكاح الا بولي وشاهدي عدل رواه البيهقي
"Hakuna ndoa bila ya Walii na Mashahidi wawili waadilifu." [Imepokewa na Al-Bayhaqiy].
2. Kufanya sherehe kwa kuwakusanya watu kwa ajili ya Karamu ya Harusi, amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم):
رواه البخاري ومسلم أولم ولو بشاة
"Kusanya watu kwa ajili ya chakula cha harusi japo kwa kuchinja mbuzi mmoja." [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Musilm].
Ndio maana kuhudhuria watu katika sherehe ni jambo la wajibu na si khiyari kutokana na agizo la Mtume (صلى الله عليه وسلم).
Imepokewa na Ibn 'Umar ( رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ ) kwamba Nabii wa Allaah (صلى الله عليه وسلم):
Amesema:
إِذَا دُعِىَ أَحَدُكُمْ إِلَى وَلِيمَةِ عُرْسٍ فَلْيُجِبْ. رواه مسلم
"Atakapoitwa mmoja wenu katika karamu ya harusi basi na aitikie." [Imepokewa na Muslim].
Wanachuoni wanaona kutokana na Hadiyth hii ni wajibu kuitikia mwaliko wa harusi isipokuwa endapo harusi yenyewe ina maovu (munkarat) katika hali hiyo itakuwa haifai kuhudhuria ila kwa yule ambae ana uwezo wa kuzuia munkari wowote utakaofanyika harusini.
Na endapo aliyealikwa hakujua kwamba harusi hiyo ina munkar na akashtukiziwa na munkar kama vile kupigwa miziki wakati wa kula chakula cha walima, basi na azuie akiweza kama hakuweza basi itamlazimu kuondoka haraka, kwa sababu kuendelea kukaa na kula ni kuwapa nguvu na ushindi waovu.
Na hii ndio kauli yenye nguvu ya Wanachuoni wa Madhehebu wa Kishafii kama ilivyo kwenye Kitabu: Al-Haawil Kabiyr juz. 9 uk. 563, na Al-Mughnil Muhtaaj juz. 3 uk. 247, na Asnal-Matwaalib juz. 3, uk. 226. Na pia Wanachuoni wa Madhehebu ya Kihambal, angalia Kitabu: Al-Mughniy juz. 10, uk. 198, Kashaaful Qanaa juz. 4, uk, 190, na Al-Inswaaf juz. 8, uk. 335.
Na imepokewa na Abu Hurayrah ( رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ ) kwamba Nabii wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema:
(شر الطعام طعام الوليمة، يدعى إليها من يأباها ويمنعها من يأتيها، ومن لم يجب، فقد عصى الله ورسوله) رواه مسلم
"Chakula cha shari ni kile chakula cha Harusi, ambacho hualikwa asiyependa kuhudhuria, na anaachwa yule ambae akiitwa anaitikia wito, na yeyote yule ambae amealikwa na hakuitikia basi atakuwa amemuasi Allaah na Mtume Wake." [Imepokewa na Muslim).
Itakuwa si wajibu kuitikia mwito huo endapo aliyealikwa ana udhuru wa kishari'ah kama vile kuumwa au safari n.k.
3. Imesuniwa pia kuitangaza ndoa kwa njia ya kuwaruhusu wanawake tu, kupiga dufu na kuimba nyimbo halali na sio kupiga ngoma kama wanavyofanya baadhi ya wanawake. Amesema Mtume (صلى الله عليه وسلم):
رواه الترمذى فصل ما بين الحرام والحلال الدف والصوت
"Kinachotenganisha Halali na Haramu ni kupigwa dufu na kuimba (katika harusi)." [Imepokewa na At-Tirmidhiy].
Amesema Mwanachuoni Ibn Qudaamah katika kitabu chake cha Al-Mughniy:
"Inapendeza kuitangaza ndoa na kupigia dufu."
Na amesema Imaam Ahmad: "Na inapendeza kuidhihirisha ndoa na kupigia dufu mpaka itangazike na ijulikane."
Na anasema Mwanachuoni Ibn Hajar:
"الأصل التنَزُّه عن اللعب واللهو، فيقتصر على ما ورد فيه النص وقتاً وكيفية، تقليلاً لمخالفة الأصل"
"Na asili ni kujiepusha na michezo na mambo ya upuuzi,na kubaki tu na kile kilichokuja kwenye Dalili (Naswi) kwa wakati (wa kutekeleza) na jinsi ya (kutekeleza) ili kupunguza kupingana na asili." Fat-hu-Baariy juz. 3, uk. 267.
Ifahamike kwamba Wanaume hawakuruhusiwa kwa hali yoyote kupiga aina yoyote ya ngoma au ala ya muziki iwe ni kwenye harusi au nje ya harusi.
Si Mtume (صلى الله عليه وسلم) wala Swahaba yeyote aliyewahi kupiga ngoma ya aina yoyote zama za Mtume (صلى الله عليه وسلم) na hata baada ya kufa kwa Mtume (صلى الله عليه وسلم). Ama yanayofanywa leo na Wanaume juu ya hilo ni kinyume na mafunzo ya Uislam.
Amenukuu Mwanachuoni wa Ki-Shaafi'iy Ibn Hajar Al-Haithamiy kauli ya Wanachuoni wema waliopita wakisema:
"Kupiga dufu hakuwi halali isipokuwa kwa wanawake kwa sababu ni asili yao na katika matendo ya wanawake na amewalaani Mtume (صلى الله عليه وسلم): wanaume wanaojifananisha na wanawake." [Kaffu Riaa uk. 96].
Na kwenye Hadiyth ya Mtume (صلى الله عليه وسلم) iliyopokewa na Ibn 'Abbaas (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) amesema:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ قَالَ لَعَنَ النَّبِىُّ - صلى الله عليه وسلم - الْمُخَنَّثِينَ مِنَ الرِّجَالِ،وَالْمُتَرَجِّلاَتِ مِنَ النِّسَاءِ وَقَالَ « أَخْرِجُوهُمْ مِنْ بُيُوتِكُمْ رواه البخاري
"Amewalaani mtume wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) wanaume wanaojifananisha na wanawake, na wanawake wanaojifananisha na wanaume na akasema (صلى الله عليه وسلم): waondoeni mwenye majumba yenu." [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
Haifai ni haramu kuhudhuria harusi au sherehe yoyote kama vile mikutano ya kisiasa n.k. ambayo ina munkari ndani yake au mahali ambapo paliandaliwa kwa ajili ya kumuasi Mola. Ni haramu kuhudhuria harusi yenye aina yoyote ya muziki, ngoma au taarab, au ulevi, mirungi na aina yoyote nyingine za maasi isipokuwa endapo utaweza kuondoa Munkari huo.
Amesema Allah (سبحانه وتعالى):
وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللَّـهِ يُكْفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلَا تَقْعُدُوا مَعَهُمْ حَتَّىٰ يَخُوضُوا فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ ۚ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا
"Naye Amekwishakuteremshieni katika Kitabu kwamba mnaposikia Aayah za Allaah zinakanushwa na zinafanyiwa istihzai, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengineyo. Au sivyo mtakuwa kama wao. Hakika Allaah Atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika (moto wa) Jahannam." [An-Nisaa: 140].
Amesema Mwanachuoni Al-Qurtubiy katika kufasiri Aayah hii:
"Hii imeonyesha dalili ya wajibu wa kujiweka mbali na watu wenye kufanya maasi endapo atadhihirisha miongoni mwao munkari (uovu) kwani ambae hajitengi nao, basi atahesabiwa ameridhia tendo lao hilo, na kuridhia kufru na ukafiri. Hivyo kila mwenye kukaa kikao cha maasi na akawa hakukataza maasi hayo atakuwa pamoja nao katika mizani sawa kwa sawa.
Na itampasa awakataze pindipo wataanza kuzungumza au kufanya maasi. Na ikiwa hatoweza kuwakataza basi itampasa aondoke kwenye majlis yao ili asije akawa katika wahusika wa aya hii (mtu wa motoni)."
Na imepokewa na Swahaba Thaabit bin Adhw-Dhwahaak akisema:
أنَّ رَجُلا نَذَرَ أنْ يَنْحَرَ إبِلاً بِبُوَانَةَ، فسأل النبي - صلى الله عليه وسلم - فقال له: «هَلْ كَانَ فِيهَا وَثَنٌ مِنْ أوْثَانِهم؟».
قال: لاَ. قالَ: «فهَلْ كَانَ فِيهَا عِيدٌ مِنْ أعْيَادِهِمْ؟» قال: لاَ. قالَ: «فأوْفِ بِنَذْرِكَقال: فأوف بنذرك، فإنه لا وفاء لنذر في معصية الله، ولا فيما لا يملك ابن آدم)»رواه أبو داود
"Mtu mmoja aliweka nadhiri ya kuchinja ngamia sehemu inayoitwa Bawana. Mtume (صلى الله عليه وسلم) akauliza na akasema: Je, kulikuwa hapo na mzimu katika mizimu ya kijahiliyah ikiabudiwa? Akasema, Hapana. Akasema Mtume (صلى الله عليه وسلم): Je, kuna sherehe za sikukuu katika sikukuu zao? Akasema: Hapana. Akasema Mtume (صلى الله عليه وسلم): Tekeleza nadhiri yako kwani hakuna kutekeleza Nadhiri katika kumuasi Allaah, wala kwa kile asichomiliki Mwanadamu." [Imepokewa na Abu Daawuwd].
Amesema Imaam Ibn Baaz katika kusherehesha Hadiyth hii:
"Katika Hadiyth hii kuna dalili ya kukatazwa kufanya ibada katika athari za Washirikina kwa sababu hizo ni sehemu Alizoharamisha Allaah kutokana na vitendo vya shirki na maasi yanayofanywa humo. Na Hadiyth japo imezungumzia nadhiri tu lakini itabeba maana pana kwamba kila ibada inayokusudiwa Allaah haitofaa kufanywa katika maeneo maovu ambayo yamegeuzwa kuwa ni sehemu za kumkasirisha Mola Aliyetukuka." [Fat-hul-Majiyd uk. 134].
Kwa maana hiyo basi haitofaa kwa Muislam kufanya sherehe za ibada ya harusi katika mahali au kumbi ambazo zimeaandaliwa hasa kwa ajili ya kumuasi Mola kama vile kumbi za sinema, mabaa, kanisani, kumbi za Mabaniani (Hindu Mandal), kumbi za vyama vya kisiasa za Kitwaghuti k.m. CCM HALL n.k.
Na miongoni mwa munkarati inayopatikana katika Harusi ni pamoja na: Bwana harusi kutolewa kwenye Ukumbi (Hall) mbele ya wanawake ajnabiyah ambao wengi wao hawakuvaa nguo za stara, na kulishana keki hadharani, au kupigana mabusu, na kupigwa picha hatimae kusambazwa kwa ndugu na marafiki,na kuangaliwa picha hizo na wanaume ajnabiyah, yote haya ni haraam.
Kwa mujibu wa mafunzo haya yaliyotajwa hapo nyuma, Mtume (صلى الله عليه وسلم), hakusita kuzuia ovu (munkar) pindipo akiuona au kuusikia. Siku moja alisikia wasichana wakiimba harusini wimbo wenye maneno yafuatayo:
كما في صحيح البخاري: " وفينا رسول الله يعلم ما في غد فسمعها رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال لها: دعي هذا وقولي غيره
"Na tunaye hapa Nabiii anayejua yatokeayo kesho." Akasema Mtume (صلى الله عليه وسلم) kwa kuwakemea "Acheni maneno haya, na semeni yale mliokuwa mkiyasema kabla ya hapo." [Imepokewa na Al-Bukhaariy].
Sababu ya kukemea Mtume (صلى الله عليه وسلم): maneno haya ni ile kumbebesha Mtume (صلى الله عليه وسلم) sifa ambazo si zake, kwani hakuna nafsi yoyote inayojua kitakachotokea kesho kwa hakika isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى) peke Yake.
Nae Mtume (صلى الله عليه وسلم) mara nyingine amesikika akisema:
(ومن كان يؤمن بالله واليوم الآخر فلا يجلس على مائدة يدار عليها الخمر)
"Mwenye kumuamini Allaah na siku ya Mwisho basi na asikae kwenye chakula ambacho huzungushiwa ulevi." [Imepokewa na Ahmad].
Kuna wema waliopita walielewa msimamo wa Mtume (صلى الله عليه وسلم): kwamba haifai kwa ujumla kuhudhuria mahali ambapo pana munkar iwe harusini au penginepo.
Inasimuliwa kwamba Abu Mas'uwd 'Uqbah bin 'Aamir, mtu mmoja alimuandalia chakula kisha akaalikwa akasema (kumwambia aliyemualika):
"Je, katika nyumba ulionialika kuna sanamu? Akasema yule mtu Naam." Akakataa Abu Mas'uwd kuingia mpaka lilipovunjwa lile sanamu ndipo akaingia.
Vile vile amenukuliwa Imaam Al Awza'iy akisema:
"Hatuiingii kwenye chakula cha Harusi ambapo hupigwa ndani yake ngoma au chombo chochote cha muziki."
Ndugu Muislam, je wewe ni katika wafuasi na wapenzi wa Mtume (صلى الله عليه وسلم) basi kama hivyo ndio sahihi basi huna budi kutekeleza mafunzo ya (صلى الله عليه وسلم) bila ya kujali lawama ya wanaadamu. Waislam wengi leo hii wameacha mwongozo huu kwa sababu zifuatazo:
1. Ujinga uliobobea katika mambo ya dini, watu wameshughulishwa mno na dunia na hawana wakati wa kujifunza dini yao.
2. Jamii ya Kiislam kutokuwa na viongozi wema ambao ni mfano wa kuigwa, Mashekhe wengi wanakwenda na watu, hawataki kukemea maovu wasije wakakasirisha watu na kupoteza maslahi yao na umaarufu wao.
3. Sifa ya "Qawwaamah" imepotea kwa Wanaume wengi, Wanawake ndio wasimamizi siku hizi wa mambo ya Wanaume, ratiba za harusi siku hizi hupangwa na Wanawake na Wanaume ni wenye kutii tu bila ya kujali ratiba hiyo ina kheri au shari.
4. Tumche Mola wetu turudini katika mwongozo wa Bwana Mtume (صلى الله عليه وسلم) tutafuzu.
Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا
"Mwenye kumtii Allaah na Mtume huyo ndiye amefuzu (ushindi mkubwa)." [Al-Ahzaab: 71].
Na bora ya uongofu ni wa Bwana Mtume (صلى الله عليه وسلم) yeye ndiye anayestahiki kuigwa kwa kila kitu na tusijibebeshe mila za Makafiri tutaangamia.
No comments:
Post a Comment