Thursday, February 21, 2013

SWALAH - 1 - Maana Ya Swalah Na Kuwajibika Kwake

e

SWALAH - 1 - Maana Ya Swalah Na Kuwajibika Kwake


 

Maana Ya Swalah Kilugha
 
Ni du'aa kama Anavyosema  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 ((خُذْمنْ أَمْوَلِهمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ و تُزَكِّيهِمْ بِهَا و صَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صلواتك سَكَنٌ لَّهُمْ وَ آللّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ))
((Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe kwa ajili ya hizo (sadaka zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele ya Allaah) na uwaombee du’aa. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu na Allaah ni Mwenye kusikia Mwenye kujua)) [At-Tawbah: 103]
 Hadiyth ifuatayo inathibitisha pia maana hiyo:
 
عن أبي هريرة -رضي الله عنه- قال: قال رسول الله -صلى الله عليه وسلم: ((إذا دعي أحدكم فليجب فإن كان صائمًا فليصلِّ و إن كان مفطرًا فليطعم)) أخرجه مسلم         
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Akialikwa mmoja wenu aitike (mwaliko), ikiwa amefunga  (Swawm) awaswalie (yaani aombe (du'aa kwa waliomualika), akiwa hakufunga basi ale (chakula)))[Muslim]  [Inamaanisha awaombee du'aa ya maghfirah, baraka na kheri)
 
Swalah kutoka kwa Allaah ni sifa njema na kutoka kwa Malaika ni du'aa kama Anavyosema:
((إنَّ اللَّهَ وَ مَلاَئِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى آلنَّبِيِّ يَا أَيُّهَا آلَّذِينَءامَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَ سَلِّمُوا تَسْلِيمًا))
((Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni (muombeeni) na mumsalimu kwa salamu)) [Al-Ahzaab: 56]
Abu 'Alyah amesema: Swalah ya Allaah ni kumsifu mja kwa Malaika Wake na Swalah ya Malaika ni du'aa.
Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) amesema: "Wanawaswalia" maana wanawabarikia"  
Vile vile Swalah kutoka kwa Allaah ni Maghfirah (msamaha) au Baraka. Swalah kwa maana ya Maghfirah nikutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 ((أُوْلئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَواتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَ رَحْمَةٌ وَ أُوْلئِكَ هُمُ آلْمُهْتَدُونَ))
((Hao juu yao zitakuwa maghfira zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka))[Al-Baqarah: 157]
Na kama ilivyosimuliwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alisema:
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى آل أَبِي أَوْفَى
Allahumma Swalli ‘alaa Aali Abi AwfiyAkimaanisha ‘Ee Mola wangu wasamehe jamaa wa Abu Awfiy’.  
Hivyo hapa Swallah ina maana ya Maghfirah (msamaha).
 
 
 
Maana Swalah Kishari'ah
 
Ni kumuabudu Allaah kwa kauli na vitendo maalumu na khaswa (pekee) vinavyoanza na Takbiyr (Allaahu Akbar) na kumalizika na Tasliym (kutoa salam).
Na imeitwa Swalah kwa sababu inahusiana na du'aa katika kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tunaposimama, tunaporukuu, tunaposujudu na tunapokaa, hivyo Swalah nzima ni du'aa.
 
 
Hukumu Ya Swalah
 
Swalah ni fardhi kwa kila Muislamu mwenye akili timamu, aliyebaleghe kutokana na dalili kutoka katika Qur-aan:
   ((وَمَا اُمِرُواْ إِلاَّ لِيَعْبُدُواْ آللّهَ مُخْلِصِينَ لَهُ آلدِّينَ حُنَفَآءَوَ يُقِيمُواْ آلصَّلاَةَ وَ يُؤْتُواْ آلزَّكَاةَ وَ ذَلِكَ دِينُ آلْقَيِّمَةِ))
((Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allaah kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike Swalah, na watoe Zakaah. Na hiyo ndiyo Dini madhubuti))[Al-Bayyinah: 5]
   ((إِنَّآلصَّلاَةَ كَانَتْ عَلَى آلْمُؤْمِنِينَ كِتابًا مَّوْقُوتًا))
((Kwani hakika Swalah kwa Waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu)) [An-Nisaa: 103]
Ama katika Sunnah ni kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomtuma Mu'aadh Bin Jabal (Radhiya Allaahu) kupeleka ujumbe Yemen kwa kumwambia: ((…na wafundishe kwamba Allaah Amewafaridhisha Swalah tano kila siku…)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
Vile vile,
  عبدالله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم (( بُنِـيَ  الإِسْلاَمُ علـى خَمْسٍ: شَهادَةِ أنْ لا إِلٰهَ إلا الله وأنَّ مُـحَمَّداً رَسُولُ الله وإِقامِ الصَّلاَةِ وإِيتاءِ الزَّكاةِ وَحَجِّ البَـيْتِ وَصَوْمِ رَمَضَانَ)) البخاري
Kutoka kwa 'Abdullaah ibn 'Umar ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uislamu umejengeka kwa matano; Kushuhudia (na kukiri kwa moyo)  kwamba hakuna Mola Apasaye kuabudiwa (kwa haki) isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allaah na kuswali (Swalah tano), kutoa Zakaah, kuhiji katika Nyumba (Makkah) na kufunga (mwezi wa) Ramadhaan)) [Al-Bukhaariy]
Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazothibitisha kuwajibika kwa Swalah. Ama mwanamke mwenye hedhi na aliye katika nifaas hawawajibiki kuswali kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  
 
((Kwani sio kweli kwamba mwanamke anapokuwa katika hedhi haswali wala hafungi?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
 

No comments: