ASSALAAM ALAYKUM
KISA:
Swahaba aliyeitwa Julaybiyb alijulikana sana kuwa alikuwa ni mtu duni
asiyemiliki mali na hakuwa ni mzuri kwa sura na umbo, na alikuwa ni
mtu wa kuchekesha watu. Kwa hivyo hakuna aliyetaka kumuozesha binti
yake. Mtume (S.A.W) alimuuliza Julaybib kama anataka kuoa, naye
akamjibu: "Ewe Mjumbe wa Allah, nani atakayekubali nimuoe mimi?
Sina nyumba wala mali wala chochote katika mapambo ya dunia".
Mtume (S.A.W) akamtuma mtu mmoja aende nyumba ya Answaariy fulani
ambao walikuwa ni familia yenye kujulikana kwa kabila lao maarufu
kubwa lenye kujulikana kwa heshima na wenye hali nzuri. Alipopiga
hodi, alifungua mlango mama wa binti huyo. Swahaba akamjulisha kuwa
ametumwa na Mtume kuleta posa kwa binti yake.
Mama huyo alifurahi sana kudhania kwamba Mtume (S.A.W) ndiye anayetaka
kumposa binti yake. Swahaba Alipomjulisha kuwa sio kwa ajili ya Mtume
(S.A.W) bali ni kwa ajili ya Julaybiyb, mama huyo alisema: "Nani?
Julaybib? Hapana! Hatumuozeshi yeye binti yetu!".
Mara yule binti alisikia mazungumzo hayo akaja kuuliza vizuri: "Nani
anayetaka kuniposa?" Mama mtu akamuelezea kuwa Mtume (S.A.W) amemtuma
mtu aje kumposa yeye kwa ajili ya Julaybiyb.
Binti huyo alimwambia mama yake: "Vipi mama unakataa amri ya Mtume
(S.A.W) Fuata amri yake kwani hakuna kitakachonidhuru". (Katika usemi
mmoja ni kwamba hapo hapo Aayah ifuatayo iliteremshwa [Ibnu Kathiyr
7:692-694]) na katika usemi mwingine aliwaambia wazazi wake:
"Hamkusikia kauli ya Allah (S.W)
(وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ
وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ
وَمَن يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا)
(Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari
katika jambo, Allah na Mtume Wake Wanapokata shauri katika jambo lao.
Na mwenye kumuasi Allah na Mtume Wake basi hakika amepotea upotofu
ulio wazi)[Al-Ahzaab:36]
Ikabidi wamuozeshe binti yao kwa Julaybiyb. Kisha katika vita fulani
alitoka Mtume (S.AW) na Maswahaba miongoni mwao ni Julaybiyb na baada
ya ushindi wa vita hivyo, Mtume (S.A.W) aliwauliza Maswahaba kabla ya
kurudi: (Je, kuna mtu aliyekosekana?)
Wakataja baadhi ya Maswahaba waliokosekana kisha Mtume (S.A.W)
akawauliza tena wakasema: "Hakuna mtu mwingine aliyekosekana: Lakini
Mtume (S.A.W) akasema: (Lakini mimi naona kwamba Julaybiyb
amekosekana) yaani hayupo na sisi.
(Nendeni mkamtafute miongoni mwa waliouliwa). Wakaenda Maswahaba
kumtafuta wakamkuta ameuawa akiwa karibu yake makafiri saba ambao
aliwahi kuwaua yeye Julaybiyb. Maswahaba wakamjulisha Mtume (S.A.W)
ambaye alikwenda na kusimama karibu naye kisha akasema: (Ameua saba
kisha wakamuua. Yeye ni wangu na mimi ni wake).
Alisema hivyo mara mbili au tatu, kisha Mtume (S.A.W) akambeba kwa
mikono yake na kwenda kumzika. Na akamuombea Du'aa mke wake:
(الَّلهُمَّ، صَبَّ عَلَيْهَا [الخير] صَبَّا، وَلاَ تَجْعَل عَيْشَها كَدَّا)
(Ewe Allah, Mjaze kheri (nyingi) zilizojaa na Usimjaaliye maisha yake
kuwa ni ya shida [tabu na mashaka]
Imesemekana kwamba hakuweko mjane aliyekuwa ana maisha mema kama
maisha ya mke wa Julaybiy (R.A)
[Kisa kimesimuliwa na Imaam Ahmad Muslim na An-Nasaaiy]
Ndugu waislamu Kisa Hiki kimetufunza nini? wewe Binafsi. Funguka:
No comments:
Post a Comment