|
"SABABU KUBWA ZA KUWA WANAWAKE WACHACHE PEPONI"
Kama inavyojulikana Mtume S.A.W. alipokuwa katika safari yake ya usiku wa Israa alibahatika kuoneshwa Moto wa Jahannam akaona watu walio wengi zaidi ni wanawake. Na wakati alipowaona idadi yao ni kubwa alishangaa na kuuliza sababu yake na akajibiwa kama tutakavyoona katika Hadithi iliyopo hapo chini. Hadithi iliyopokelewa na Abu Said Al-Khudry R.A.A. na iliyotolewa na Muslim, Mtume S.A.W. kasema, "
"Enyi jamii ya wanawake! Toeni sadaka, kwani mimi nimekuoneni nyinyi zaidi watu wa Motoni. Tukasema "Na kwa nini ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akajibu akasema "Mnazidisha (kuitamka) laana na mnakanusha fadhila na ihsaani za waume zenu."Pia katika Hadithi nyingine Mtume S.A.W. alipoona Motoni idadi kubwa ya wanawake aliuliza sababu zilizowafanya wawe humo akajibiwa,
"Niliona wengi wa watu wake wanawake nikasema "Wana nini?" Ikasemwa, "Vimewashughulisha vyekundu viwili: Dhahabu na zaafarani (yaani nguo za rangi mbalimbali)." Kama inavyoonesha katika hizo Hadithi mbili zilizopo hapo juu, sababu kubwa ya wanawake wengi kuwa Motoni ni kule kughilibika kwao na dunia kwa kujishughulisha na kupenda mapambo ya aina tofauti na kutaka kuonekana na watu au kuonesha watu ikiwa ni pamoja na kudharau waume zao na kuitamka laana kwa wingi. Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas R.A.A. na iliyotolewa na Bukhari, Mtume S.A.W. kasema, "
"Nimeoneshwa Moto tahamaki (nikaona) wengi wa watu wake ni wanawake wanaokanusha." Ikaulizwa "Jee, wanamkanusha Mwenyezi Mungu?" Akasema "Wanakanusha waume (zao) na wanakanusha ihsani. Lau ukimfanyia ihsani mmoja wao mwaka mzima kisha akaona kitu kutoka kwako (cha kumchukiza) atasema "Sikuona kwako kheri yoyote ile." Pia Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar R.A.A. na iliyotolewa na Muslim na Ibn Maajah, Mtume S.A.W. kasema, "
"Enyi kundi la wanawake! Toeni sadaka na zidisheni kuomba maghufira (msamaha). Kwa hakika mimi nimekuoneni nyinyi zaidi watu wa Motoni." Mwanamke mmoja mwenye akili miongoni mwao akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Na vipi sisi tukawa wengi watu wa Motoni?" Akajibu, "Mnazidisha (kuitamka) laana na mnakufuru fadhila na ihsani za waume zenu. Sikuona waliopungukiwa akili, dini na maarifa zaidi kuliko nyinyi." Akasema (mwanamke) "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa nini tukapungukiwa akili na dini? Akajibu (Mtume S.A.W.), "Ama mmepungukiwa akili kwa sababu ushahidi wa wanawake wawili ni sawasawa na ushahidi wa mwanaume mmoja na huko ndiko kupungukiwa akili. Na mnakaa masiku hamsali na mnafungua (mwezi wa) Ramadhani na hii ndio kupungukiwa dini."
Wabilahi Toufiq
|
No comments:
Post a Comment